Sunday, April 7, 2013

ABIDAL AREJEA RASMI UWANJANI.

KWA mara ya kwanza beki wa klabu ya Barcelona Eric Abidal amerejea uwanjani toka alipofanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini jingine Aprili mwaka jana wakati alipocheza dakika 20 za mwisho katika mchezo wa La Liga ambao timu yake ilishinda kwa mabao 5-0 dhidi ya Real Mallorca. Abidal mwenye umri wa miaka 33, alifaulu vipimo na kurejea kufanya mazoezi na wenzake mwezi uliopita, ambapo mashabiki wa Barcelona walimpokea kwa kumpigia makofi wakati anabadilishana na Gerrard Pique akitokea benchi katika dakika ya 70 ya mchezo huo. 
Mara baada ya mchezo huo Abidal alimshukuru binamu yake kwa kujitolea kumpa sehemu ya ini lake ambalo ndio hilo limemsaidia kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya kukaa nje ya uwanja kwa mwaka mmoja. Abidal amesema bila binamu yake huyo asingeweza kuwepo hapo alipo hivi sasa hivyo ni siku muhimu sana kwake. Ujio wa Abidal ni ahueni kwa Barcelona ambao kwasasa wanamatatizo ya kukosa mabeki wake mahiri ambao ni majeruhi akiwemo Carlos Puyol, Javier Mascherano na Adriano.

No comments:

Post a Comment