Wednesday, April 17, 2013

AGUERO AMUOMBA RADHI LUIZ.

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester City, Sergio Aguero amemuomba radhi beki wa Chelsea David Luiz kwa mchezo mbovu aliomchezea wakati timu hizo zilipokutana katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA Jumapili iliyopita. Katika mchezo huo ambao Chelsea walipoteza kwa kufungwa mabao 2-1, walizawadiwa mpira wa adhabu baada ya Aguero kumuingilia vibaya Luiz lakini mwamuzi hakutoa kadi yoyote kutokana na tukio hilo. Baada ya mchezo huo Luiz alimtaka Aguero kumuomba radhi kitendo ambacho mshambuliaji huyo Muargentina alikifanya Jana kwa kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter. Katika ujumbe wake Aguero alikiri kumchezea vibaya Luiz na kumuomba radhi na mchezaji huyo naye alijibu kwa kukubali kumsamehe nyota huyo na kumsifu kwa ushujaa wa kukiri kosa. Chama cha Soka cha Uingereza-FA Jumatatu kilidai kuwa hakitatoa adhabu yoyote kwa Aguero kwasababu mwamuzi Foy aliona sehemu ya tukio hilo na kutoa adhabu.

No comments:

Post a Comment