Saturday, April 27, 2013

BENCHI LAMKIMBIZA KOLO TOURE MAN CITY.

BEKI wa kimataifa wa Ivory Coast na klabu ya Manchester City, Kolo Toure amethibitisha kuwa anatarajia kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu lakini hakuweka wazi timu atakayokwenda akitoka hapo. Toure mwenye umri wa miaka 32 alisajiliwa akitokea Arsenal kwa ada ya paundi milioni 16 lakini amekuwa hapati namba katika kikosi cha City baada ya kucheza mechi 12 pekee katika msimu wa mwaka 2012-2013 huku kukiwa hakuna uhakika wa kuongezewa mkataba mwingine. Toure amesema ni miaka minne toka atue City ikiwemo misimu miwili mizuri ambayo alikuwa akicheza mara kwa mara lakini anaona muda wake wa kuwepo umekwisha baada ya kusubiria kupewa mkataba mwingine kwa kipindi cha miezi miwili bila mafanikio. Amesema ni muda wa kuwaza hali yake ya mbele ingawa familia yake wakiwemo watoto wanaupenda mji huo na kudai pia hana mpango wa kutoka nje ya Uingereza kwasababu ndio nchi pekee ya Ulaya anayojua tamaduni zake toka atoke kwao Ivory Coast mwaka 2002. Klabu ya Monaco ya Ufaransa imeonyesha nia ya kutaka sahihi ya nyota huyo lakini wamedai kuwa hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanza na wakala wa mchezaji huyo.

No comments:

Post a Comment