Thursday, April 18, 2013

MASHABIKI WAJIPONZA MISRI.

MABINGWA wa nchini Misri klabu ya Zamalek, inatarajia kucheza mechi yake ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika katika uwanja mtupu jijini Cairo mwishoni mwa wiki hii baada ya vurugu za hivi karibuni zilizopelekea mashabiki kuzuiwa kabisa. Wizara ya mambo ya ndani ya nchi iliruhusu mashabiki wapatao 3,000 katika baadhi ya mechi za mashindano ya vilabu barani Afrika kwa vilabu vya Zamaleki na Al-Ahly ambazo zote zinatoka mjini Cairo. Lakini pamoja na mashabiki hao kuruhusiwa kwa uchache katika Uwanja wa Borg El Arab ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 90,000 kumekuwa na vurugu mbalimbali kwenye baadhi ya mechi. Mashabiki wa Zamalek walionekana kupagawa na kuanza kushangilia kwa kuvunja viti hovyo uwanjani baada ya timu yao kuishindilia timu ya Gazelle ya Chad kwa mabao 7-0 kitu ambacho kilistaajabisha watu wengi na kuzua hofu kama matokeo hayo yangekuwa kinyume chake. Kwa upande wa Al Ahly mashabiki wao walikuwa wakirusha vitu uwanjani wakati wa mchezo baina yao na Tusker ya Kenya mchezo ambao wenyeji walishinda kwa mabao 2-0. Matukio hayo ndio yamepelekea watu wa usalama kuhofu usalama kama mashabiki wakiruhusiwa kuingia katika mechi zingine hivyo kuamua kuzuia kabisa mpaka hapo watakapojiridhisha kwamba hali imetulia.

No comments:

Post a Comment