Tuesday, April 16, 2013

NITAENDELEA KUKIMBIA MARATHON PAMOJA NA YALIYOTOKEA BOSTON - KORIR.

BINGWA wa mashindano ya riadha ya mbio ndefu ya Boston 2012 na pia mbunge wa serikali mpya ya Kenya, Wesley Korir ameeleza hofu yake baada ya kusikia mlipuko ulioua katika mbio za Boston mwaka huu ambazo alimaliza katika nafasi ya tano. Milipuko miwili ilitokea karibu na eneo la kumalizia mbio hizo na kuua watu watatu na wengine zaidi ya 140 kujeruhiwa ikiwa imepita saa mbili toka washindi wa mbio hizo walipomaliza. Korir amesema kama tukio hilo lingetokea saa mbili kabla pengine angekuwa mmoja wa wahanga. Mbunge huyo ambaye anatoka katika jimbo la Cherangany amesema wakati tukio hilo linatokea walikuwa wakishangilia ushindi wa mwanadada wa Kenya Rita Jeptoo ambapo furaha yote ilikatizwa na mlipuko uliotokea. Korir amesema pamoja na milipuko hiyo na shughuli zake mpya za kisiasa ataendelea kukimbia mbio ndefu hata kama zitaandaliwa tena jijini Boston mwaka ujao.

No comments:

Post a Comment