Monday, April 22, 2013

SUAREZ ALIMWA FAINI NA LIVERPOOL BADO YA FA INAMNGOJA.

MSHAMBULIAJI mkorofi wa Liverpool, Luis Suarez amepigwa faini na klabu yake hiyo na hela zitapelekwa kusaidia familia zilizoathirika na tukio la Hillsborough kufuatia mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay kumng’ata meno beki wa Chelsea Branislav Ivanovic. Suarez alifanya tukio hilo la kushangaza la kumng’ata meno katika mkono wa kulia wa Ivanovic katika mchezo baina ya timu hizo uliochezwa jana ambao walitoka sare ya kufungana mabao 2-2 katika Uwanja wa Anfield. Kuna uwezekano mkubwa Suarez akapewa adhabu nyingine na Chama cha Soka cha Uingereza-FA ambao bado wanachunguza tukio lakini Liverpool tayari wameshamuadhibu nyota huyo ambaye atatakiwa kutoa faini ambayo ataipeleka kwa familia za watu 96 waliofariki dunia katika vurugu za mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA kati ya timu hiyo na Hillsborough mwaka 1989. Jumatatu iliyopita ilifanyika kumbukumbu ya miaka 24 toka kutokea kwa tukio hilo katika Uwanja wa Anfield shughuli ambayo Suarez na wachezaji wenzake wa Liverpool walihudhuria. Suarez tayari ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akimuomba radhi Ivanovic, mashabiki na wachezaji wenzake kwa tukio hilo ambalo hata mwenyewe alikiri kuwa ni tabia isiyokubalika.

No comments:

Post a Comment