Tuesday, April 30, 2013
UNITED WAPEWA MWAMUZI WAO MECHI DHIDI YA CHELSEA.
MWAMUZI Howard Webb ameteuliwa kuchezesha mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza kati ya Manchester United na Chelsea utakaochezwa katika Uwanja wa Old Traford Jumapili. Webb mwenye umri wa miaka 41 ambaye alichezesha mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2010 sio mgeni katika kuchezesha mechi zenye utata baina ya vilabu hivyo vikubwa ambavyo vyote vimekuwa vikilalamikia baadhi ya maamuzi yanayotolewa naye. Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Ryan Babel aliwahi kutuma picha katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akimuonyesha Webb ametinga jezi ya United kufuatia kufingwa na timu hiyo bao 1-0 Januari mwaka 2011 huku akiandika ujumbe mkali wa kumponda. Hatua hiyo ilipelekea Babel kuwa mchezaji wa kwanza kuadhibiwa na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa matumizi mabaya ya mtandao wa kijamii. Webb pia alishakwaruzana na meneja wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho kufuatia kukataliwa kwa bao la Salomon Kalou katika mchezo dhidi ya Blackburn Rovers mwaka 2007 ambapo Mourinho alimtaka mwamuzi huyo kuomba radhi kwa kosa alilofanya. United wameshinda mechi 13 na kupoteza moja tu katika mechi 15 za ligi kuu ambazo Webb amechezesha Old Traford.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment