Sunday, May 12, 2013

MOURINHO AWAPONGEZA BARCELONA.

MENEJA wa klabu ya Real Madrid ya Hispania, Jose Mourinho amekiri kuwa Barcelona wamestahili kunyakuwa taji la Ligi Kuu ya nchi hiyo maarufu kama La Liga, kufuatia sare ya bao 1-1 iliyopata timu yake dhidi ya Espanyol jana. Katika mchezo huo Madrid walishindwa kutamba ugenini baada ya kujikuta wakitangulia kufungwa na wenyeji wao kabla ya Gonzalo Higuain kusawazisha lakini walishindwa kuongeza bao lingine ili kuhakikisha wanabakia katika mbio za ubingwa. Mourinho mwenye umri wa miaka 50 amesema anaipongeza Barcelona, makocha wao, wachezaji na mashabiki kwa kazi kubwa na yenye mafanikio waliyofanya katika msimu huu mpaka kuhakikisha wanatawadhwa mabingwa wapya wan chi hiyo. Mbali na kuipongeza Barcelona, Mourinho pia alionyesha kukasirishwa na swali aliloulizwa na mwandishi kuhusu sakata la kumuacha katika kikosi cha kwanza nahodha Iker Casillas akidai kuwa akiwa kama kocha hapaswi kutoa sababu yoyote kuhusiana na hilo. Mourinho amesema kwasasa ligi ina bingwa mpya hivyo anashangaa watu wanapozungumzia mchezaji mmoja, kwani yeye akiwa kama kocha ana uhuru wa kuchagua nani acheze na nani asicheze hivyo haoni kama swali hilo lilikuwa na maana.

No comments:

Post a Comment