Wednesday, June 5, 2013

BOLT KUTETEA UBINGWA WAKE JIJINI ROME.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi, Usain Bolt amedai kuwa na mategemeo ya kurejea katika kiwango chake bora baada ya kusumbuliwa na msuli wa paja mwezi mmoja uliopita. Bolt ambaye anashikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 100 anatarajia kushiriki michuano ya Golden Gala kesho yakiwa ni mashindano yake ya kwanza barani Ulaya kwa msimu huu. Manariadha huyo ambaye ni bingwa mara sita wa michuano ya Olimpiki amekimbia mara moja katika mbio za mita 100 kwa mwaka huu katika visiwa vya Cayman Mei 8 na kushinda mbio hizo kwa kutumia muda wa taratibu wa sekunde 10.09. Bolt amesema katika mbio hizo alitumia muda usioridhisha lakini aligundua wapi alikosea na kwenda kujifua zaidi na hivi sasa yuko fiti kurejea katika kiwango chake. Hii itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwa Bolt kukimbia katika Uwanja wa Olimpiki jijini Rome Italia ambapo mwaka 2011 alishinda kwa kutumia muda wa sekunde 9.91 na mwaka jana alishinda kwa sekunde 9.76. Bolt anashikilia rekodi ya Dunia ya mbio za mita 100 kwa kutumia sekunde 9.58 aliyoiweka katika mashindano ya dunia yaliyofanyika jijini Berlin, Ujerumani mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment