MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Misri Ahmed Hossam Hussein Abdelhamid maarufu kwa jina Mido ametangaza kutundika daruga rasmi baada ya miaka 14 ya kucheza soka la kulipwa. Mido mwenye umri wa miaka 30 alitua barani Ulaya kwa mara kwanza akitokea klabu yake ya utotoni ya Zamalek na kwenda kujiunga na Ajax Amsterdam ambapo baada ya misimu miwili aliondoka na kwenda kwenye ligi zingine barani humo kama La Liga, Ligue 1 na Serie A. Nyota huyo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa anatangaza rasmi kustaafu kucheza soka na kuwashukuru watu wote waliokuwa karibu naye katika kipindi alichokuwa akicheza haswa mashabiki wan chi yake. Mido alijulikana zaidi katika kipindi cha miaka miwili aliyochezea klabu ya Tottenham Hotspurs kwa mkopo akitokea AS Roma wakati alipoisaidia klabu hiyo kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi msimu wa 2005-2006. Toka alipoondoka White Hart Lane, Mido amepitia katika vilabu vya Middlesbrough, Wigan Athletic, West Ham United na Barnsley, lakini toka Januari mwaka huu amekuwa hana timu.
No comments:
Post a Comment