
Wednesday, July 17, 2013
HINGIS AREJEA TENA KATIKA ULINGO WA TENISI.
MWANADADA nyota wa tenisi wa zamani, Martina Hingis kutoka Switzerland anatarajiwa kurejea tena katika ulingo wa tenisi baada ya kustaafu mchezo huo mwaka 2007. Hingis mwenye umri wa miaka 32 amekubali mwaliko wa kucheza michuano ya wazi ya California ya wawili wawili akiwa sambamba na Daniela Hantuchova baadae mwezi huu. Nyota huyo ambaye amewahi kushinda mataji matano ya Grand Slam kwa mchezaji mmoja mmoja likiwemo taji la Wimbledon mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 16, Jumamosi iliyopita alichaguliwa kuwa mmoja wa wachezaji mashuhuri wa mchezo huo kuwahi kutokea. Akihojiwa kuhusiana na uamuzi huo wa kurejea uwanjani baada ya kupita kipindi kirefu, Hingis ambaye pia amewahi kushika namba moja katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanawake amesema bado anahisi kuwa na ari ya ushindani ndani ya nafsi yake. Mara ya kwanza Hingis alistaafu mchezo huo akiwa na miaka 22 baada ya kusumbuliwa na majeraha lakini alirejea tena mwaka 2006 kabla ya kustaafu tena mwaka 2007 baada ya kukutwa na chembechembe ya dawa za kusisimua misuli ingawa mwenyewe alikana tuhuma hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment