Saturday, July 20, 2013

MO FARAH AWEKA REKODI MPYA ULAYA KATIKA MBIO ZA MITA 1,500.

MWANARIADHA bingwa wa michuano ya olimpiki, Mo Farah amefanikiwa kuvunja rekodi iliyosimama kwa kipindi cha miaka 28 katika mbio za mita 1,500 iliyowekwa na Steve Cram wa Uingereza katika mashindano ya Diamond League iliyofanyika jijini Monaco. Mwanariadha huyo wa Uingereza anakuwa mtu wa sita mwenye kasi zaidi katika mbio hizo duniani akitumia muda wa dakika 3 na sekunde 28.81 huku pia muda huo ukiwa ni wa rekodi kwa bara la Ulaya. Farah ambaye ni bingwa wa olimpiki katika mbio za mita 5,000 na 10,000, alishika nafasi ya pili katika mbio hizo akiwa nyuma ya Asbel Kiprop wa Kenya ambaye alishinda kwa kuweka rekodi ya muda wa haraka zaidi duniani ya dakika 3 sekunde 37.72. Akihojiwa mara baada yam bio hizo Farah ambaye ana asili ya Somalia amesema amefurahi kushinda mbio na anajiona yuko katika kiwango kizuri kwa ajili ya mashindano ya riadha ya dunia yanayotarajiwa kuanza mwezi ujao. Kwa upande mwingine mwanariadha nyota wa mbio fupi Justini Gatlin wa Marekani amefanikiwa kushinda mbio za mita 100 kwa kutumia muda wa sekunde 9.94 huku Mmarekani mwenzake Duane Solomon akishinda mbio za mita 800.

No comments:

Post a Comment