KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amekiri kuwa mchezo wa kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN baina ya kikosi chake na timu ya taifa ya Uganda, The Cranes utakuwa mgumu lakini wamejiandaa vyema ili waweze kupata matokeo mazuri. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Poulsen amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri na kwamba wachezaji wote wako fiti wakiusubiri kwa hamu na kuwaomba mashabiki kumiminika kwa wingi Uwanja wa Taifa kesho kuishangilia timu yao. Naye Rais wa Shirikisho la Soka nchini-TFF, Leodgar Tenga amesema amezungumza wachezaji na wamemhakikishia kwamba wamejiandaa vyema na wanamatumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo.Kwa upande wa kocha wa Cranes, Milutin Sredojevic maarufu kwa jina la Micho amesema anaiheshimu Stars kutokana na ubora wake na uzoefu wa wachezaji walionao hivyo anatarajia mchezo mgumu na wenye ushindani kutoka pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment