Friday, July 12, 2013
WAJERUMANI WATAWALA MASHINDANO YA TOUR DE FRANCE.
WAENDESHA baiskeli kutoka Ujerumani wameendelea kufanya vyema katika michuano inayoendelea ya Tour de France baada ya Marcel Kittel kuibuka kidedea katika hatua ya 12 ya michuano hiyo. Kittel alifanikiwa kushinda hatua hiyo kwa kumpita kwa hatua chache Mark Cavendish wa Uingereza ukiwa ni ushindi wake wa tatu katika michuano hiyo ambayo anashiriki kwa mara ya pili. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alishinda katika hatua ya kwanza ya michuano hiyo iliyofanyika jijini Bastia na baadae kumshinda mjerumani mwenzake Andre Greipel katika hatua ya 10 jijini Saint-Malo Jumanne iliyopita. Ukiongeza na ushindi wa Greipel katika hatua ya sita jijini Montepellier pamoja na Tony Martin katika hatua ya 11 jijini Mont-Saint-Michel kunafanya waendesha baiskeli wa Ujerumani mpaka sasa kushinda hatua tano za michuano hiyo. Mchezo wa baiskeli nchini Ujerumani umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukimbiwa na wadhamini kutokana na kashfa za mara kwa mara za utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu kwa washiriki wa mashindano ya mchezo huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment