Tuesday, August 13, 2013

ABIDAL SASA ANA MATUMAINI YA KUCHEZA KOMBE LA DUNIA.

BEKI wa zamani wa klabu ya Barcelona, Eric Abidal hakuwahi kufikiria kama anaweza tena kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa wakati alipofanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini jingine lakini hivi sasa ana matumaini ya kuitumikia timu hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil. Abidal mwenye umri wa miaka 33 aliachwa na Bracelona kutokana na kiwango chake kushindwa kumshawishi kocha wa timu hiyo baada ya kupona kutokana na upasuaji aliofanyiwa April mwaka jana. Lakini baada ya kujiunga na klabu yake ya zamani ya AS Monaco kama mchezaji huru juhudi zake katika mechi za kujipima nguvu zimeonyesha kuzaa matunda baada ya kocha wa Ufaransa Didier Deschamps kumuita kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Ubelgiji. Akihojiwa na waandishi wa habari jijini Paris kabla ya kusafiri na timu hiyo kuelekea Ubelgiji, Abidal amesema hakutegemea kama anweza kufikia hatua aliyopo baada ya kukutwa na matatizo katika kipindi cha miaka miwili. Abidal aliendelea kudai kuwa kwasasa anajisikia furaha na anategemea kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu ili aweze kuitwa katika kikosi kitakachokwenda Brazil kama kocha ataona anafaa.

No comments:

Post a Comment