MCHEZAJI nyota wa tenisi, Novak Djokovic amefanikiwa kutinga hatua ya tatu ya michuano ya Kombe la Rogers inayofanyika jijini Montreal baada ya kumgaragaza Florian Mayer kwa 6-2 6-1. Ikiwa ni michuano yake ya kwanza toka alipogaragazwa na Andy Murray katika fainali ya Wimbledon mwezi uliopita, Djokovic ambaye anatoka Serbia alimuangusha mpinzani wake ambaye ni Mjerumani kwa kutumia dakika 55 pekee. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Djokovic ambaye anaongoza katika orodha za ubora wa mchezo duniani amesema amefurahishwa na ushindi huo kwani unamfanya ajiamini zaidi baada ya kupumzika kwa takribani mwezi mmoja. Kwa upande wa Rafael Nadal aliyekuwa akicheza pamoja na Pablo Anduja walifanikiwa kuwafunga David Ferrer na Feliciano Lopez kwa 6-7 6-1 katika mzungungo wa kwanza wa michuano hiyo kwa wachezaji wawili wawili. Nadal ambaye alitolewa katika hatua za mwanzoni katika michuano ya Wimbledon ameamua kushiriki michuano ya wawili wawili ili kujiweka fiti baada ya kupita miezi miwili kukosa mechi za mashindano.

No comments:
Post a Comment