MWANARIADHA nyota kutoka Uingereza, Mo Farah ameendelea kung’aa katika michuano ya riadha ya dunia inayoendelea jijini Moscow kwa kufanikiwa kuwa mwanariadha wa pili katika historia kunyakuwa medali mbili za dhahabu katika michuano hiyo na olimpiki. Farah mwenye umri wa miaka 30 alifanikiwa kumaliza katika nafasi ya kwanza katika mbio za mita 5,000 na kushinda dhahabu jana kama alivyofanya katika mbio za mita 10,000 jumamosi iliyopita. Katika mbio hizo ilikuwa ni vita kati ya Farah na Isiah Kiplangat Koech wa Kenya lakini mwingereza huyo alifanikiwa kuongeza kasi na kumpita mkenya huyo zikiwa zimebakia mita 40 kabla ya kumalizika kwa mbio hizo akitumia muda wa dakika 13 ns sekunde 26.99. Akihojiwa Farah ambaye ana asili ya Somalia amesema anajisikia fahari kushinda medali hizo na kuiwakilisha vyema nchi yake. Baadae leo mwanariadha nyota wa mbio fupi Usain Bolt wa Jamaica anatarajiwa kutetea taji lake katika fainali ya mbio za mita 200 baada ya kufanikiwa kulirejesha mikononi mwake taji la mbio za mita 100 wiki iliyopita.
No comments:
Post a Comment