Tuesday, August 13, 2013

MO FARAH AJIWEKA PAZURI KUSHINDA MEDALI MBILI ZA DHAHABU MOSCOW.

MWANARIADHA nyota wa mbio za umbali wa kati, Mo Farah kutoka Uingereza amejiweka katika nafasi nzuri ya kuibuka na medali nyingine ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia kwa kufanikiwa kufuzu fainali ya mbio za mita 5,000. Jumamosi iliyopita Farah alifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mwingereza wa kwanza kushinda mbio za mita 10,000 katika mashindano hayo yanayoendelea jijini Moscow. Farah ambaye ni bingwa matetezi wa mbio hizo za mita 5,000 alishika nafasi ya tano na kufuzu moja kwa moja kwenda fainali akitumia muda wa dakika 13 na sekunde 23.93. Kama akifanikiwa kushinda mbio za fainali zitakazofanyika Ijumaa, Farah atakuwa ameungana na Kenenisa Bekele kuwa mwanariadha wa pili kushinda medali za dhahabu ya mbio za mita 10,000 na 5,000 katika michuano ya olimpiki na dunia.

No comments:

Post a Comment