WINGA wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery amekiri kuwahi kufikiria kuihama klabu hiyo na kwenda Barcelona katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2009 lakini aliamua kuheshimu mkataba wake na kubakia. Winga huyo wa kimataifa wa Ufaransa pia alikuwa akihusishwa na kutaka kusajiliwa na Real Madrid miaka michache iliyopita lakini sasa ameweka wazi kuwa Madrid sio klabu pekee iliyokuwa ikimhitaji nchini Hispania. Ribery amedai kuwa mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Eric Abidal ambaye alikuwa akicheza chini ya Pep Guardiola akiwa Barcelona alimfuata na kumwambia suala hilo katika msimu wa 2008-2009. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alikiri kufikiria kujiunga na klabu hiyo kwa kipindi hicho kwasababu walikuwa na kikosi bora duniani. Ribery aliendelea kudai kuwa alikuwa katika kipindi kigumu kufanya uchaguzi lakini kwasababu ya umuhimu wa Karl-Heinz Rummenigge na Uli Hoeness ambaye ndiye rais wa klabu hiyo kwake aliamua kuheshimu mkataba wake na kutulia.
No comments:
Post a Comment