WINGA machachari wa klabu ya Bayern Munich, Franck Ribery ameungana na Cristiano Ronaldo na Lionel Messi katika orodha ya wachezaji watatu wa mwisho watakaogombea tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ulaya. Winga huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alitoa mchango mkubwa kwa klabu yake na kushinda michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ndio mchezaji wa kwanza kutoka klabu tofauti na Barcelona na Real Madrid kutinga hatua ya tatu bora toka tuzo hizo zilipoanza kutolewa na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA mwaka 2011. Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Messi ndiye aliyenyakuwa tuzo hiyo mwaka 2011 na kufuatiwa na kiungo mahiri wa Hispania Andres Iniesta ambaye wanacheza wote Barcelona aliyechukua tuzo hiyo mwaka uliopita. Messi na Ronaldo ndio wachezaji pekee waliofanikiwa kutinga hatua ya tatu katika kipindi cha miaka miwili mfululizo. Wachezaji wenzake na Ribery katika klabu ya Bayern ambayo ilinyakuwa mataji matatu msimu uliopita, Thomas Mueller, Arjen Robben na Bastian Schweinsteiger walikuwemo katika orodha ya wachezaji 10 iliyotangazwa mwezi uliopita. Mshindi wa tuzo hiyo atachaguliwa na jopo la waandishi wa habari za michezo kutoka kila nchi ambayo ni mjumbe wa UEFA Agosti 29 katika upangaji ratiba wa makundi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaofanyika jijini Monaco, Ufaransa.

No comments:
Post a Comment