Sunday, September 22, 2013

BAYERN, DORTMUND WAKABANA KOO BUNDESLIGA.

KLABU ya Bayern Munich imefanikiwa kuifikia Borussia Dortmund kileleni kwa kuwa na alama sawa kwenye msimamo wa Ligi nchini Ujerumani maarufu kama Bundesliga baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Schalke jana. Mabao yaliyofungwa na Bastian Schweinsteiger na Mario Mandzukic katika kipindi cha kwanza na mengine ya Franck Ribery na Claudio Pizarro katika kipindi cha pili yaliyosha kuwapa Bayern ushindi huo huku hicho kikiwa kipigo chake cha kwanza kikubwa kwa Schalke nyumbani toka mwaka 1981. Mapema jana Dortmund walipoteza rekodi yao ya asilimia mia moja kwa kutoa sare ya bao 1-1 na Nuremberg katika mechi nyingine ya Bundesliga. Bayern na Dortmund zote zina alama 16 katika mechi sita walizocheza na pia wakiwa sawa kwa tofauti ya mabao lakini Dortmund wako kileleni kwasababu wamefunga mabao mengi zaidi ya Bayern.

No comments:

Post a Comment