Tuesday, September 10, 2013

BLATTER AKIRI PENGINE FIFA ILIFANYA MAKOSA KUIPA QATAR KUANDAA KOMBE LA DUNIA 2022.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amedai kuwa pengine shirikisho hilo lilifanya makosa kuipa nchi ya Qatar uenyeji wa kuandaa michuano ya Kombe la Dunia 2022. Joto katika kipindi cha majira ya kiangazi linaweza kufikia nyuzi joto 50 katika nchi hiyo iliyopo Mashariki ya Kati. Mwenyekiti wa Chama cha Soka nchini Uingereza, Greg Dyke amewahi kukaririwa akidai kuwa itakuwa ni suala lisilowezekana kucheza katika hali hiyo na kumtaka Blatter kubadilisha michuano hiyo ichezwe katika majira ya baridi. Akihojiwa na mtandao wa insideworldfootbal kuhusu kuipa Qatar uenyeji wa michuano hiyo, Blatter mwenye umri wa miaka 77 amekiri kuwa pengine walifanya makosa katika kipindi hicho. Blatter amesema pamoja na hayo bado wanaangalia uwezekano wa kubadilisha michuano hiyo badala ya kuchezwa katika kipindi cha kiangazi ichezwe majira ya baridi kwa kuzingatia kalenda ya kimataifa katika mkutano watakaokutana mwezi ujao. Hatua inapingwa vikali barani Ulaya kwa kudai kuwa watavuruga ratiba za ligi zao kwani katika kipindi cha majira ya baridi ligi nyingi zinakuwa ziko katikati. Qatar ilishinda nchi za Korea Kusini, Japan, Australia na Marekani katika kinyang’anyiro hicho ambapo wajumbe 22 wa kamati ya utendaji wa FIFA waliichagua mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment