KIUNGO mahiri wa timu ya taifa ya Ivory Coast ambaye pia ni nahodha msaidizi, Didier Zokora ametozwa faini ya dola 20,000 na Shirikisho la Soka la nchi hiyo kwa kutoroka kambini kabla ya mechi yao ya Jumamosi ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco. Rais wa shirikisho hilo, Sidy Diallo amesema katika taarifa yake kuwa Zokora hatavaa beji ya unahodha wa timu hiyo kutokana na kitendo chake alichofanya ambacho hakikubaliki. Zokora mwenye miaka 32 ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya Trabzonspor ya Uturuki alitoroka hoteli ambayo timu ilifikia na kutokomea kusikojulikana lakini alirejea baada ya saa kadhaa baadae. Kumekuwa na tetesi kuwa Zokora aligadhabishwa kutokana na kitendo cha kuvuliwa unahodha na kupewa mshambuliaji nyota wa timu hiyo Didier Drogba ambaye alirejea katika kikosi hicho baada ya kukosekana kwa miezi kadhaa. Katika mchezo huo Ivory Coast iling’ang’aniwa sare ya bao 1-1 jijini Abidjan na Morocco ingawa pamoja na sare hiyo walifanikiwa kusonga mbele katika hatua ya mtoano.
No comments:
Post a Comment