MCHEZAJI nyota wa tenisi Roger Federer wa Switzerland amepata kipigo cha kushtusha kutoka kwa Tommy Robredo na kuvuruga matarajio ya kukutana na Rafael Nadal katika michuano hiyo ya wazi ya Marekani kwa mara ya kwanza. Federer anayeshika namba saba katika orodha za ubora duniani na Nadal anayeshika namba mbili wamewahi kupambana katika michuano yote ya Grand Slam kasoro hiyo ya Marekani na walitegemewa kukwaana katika hatua ya robo fainali. Lakini Robredo alivuruga mategemeo hayo ya watu wengi kwa kumgaraza bingwa huyo mara 17 wa mataji ya Grand Slam kwa 7-6 6-3 6-4 katika mzunguko wa nne wa michuano hiyo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Federer alionyesha kusikitishwa na kiwango alichocheza na kumpongeza mpinzani wake kwa kutumia vyema udhaifu alioonyesha kwenye mchezo na kuhakikisha anaibuka kidedea. Kwa upande wa Nadal yeye alifanikiwa kusonga mbele kwa kumgaragaza Philipp Kohlschreiber kwa 6-7 6-4 6-3 6-1 na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayochezwa jijini New York.
No comments:
Post a Comment