TIMU ya taifa ya Mexico inaweza kushindwa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwakani kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 25 kama wakishindwa kushinda mechi zao mbili ambazo ndio zitaamua hatma yao. Hali imekuwa mbaya mpaka kufikia Shirikisho la Soka la Mexico kufikiria uwezekano wa kubadilisha kocha wa timu ya taifa ambaye anatakuwa watatu katika kipindi cha siku nne. Mbali na hivyo pia vyombo vya habari vimeonyesha mapenzi madogo kwa wachezaji baada ya kupoteza mchezo dhidi ya mahasimu wao Marekani kwa kufungwa mabao 2-0 huko jijini Columbus, Ohio Jumanne. Kupoteza mchezo dhidi ya Marekani kumekuja siku chache baada ya kupoteza mchezo mwingine dhidi ya Honduras Ijumaa iliyopita hivyo kupelekea Mexico kutupwa mpaka nafasi ya tano katika timu sita za kundi la CONCACAF. Katika kundi hilo timu tatu za juu ndio zitafuzu moja kwa moja kwenda Brazil huku timu ya nne itapelekwa kucheza hatua ya mtoano na New Zealand huku mpaka sasa zikiwa zimebaki nafasi mbili pekee baada ya Marekani na Costa Rica kufuzu kwa kuchukua nafasi mbili za juu.
No comments:
Post a Comment