WAJUMBE kutoka nchi 54 ambao ni wanachama wa Shirikisho la Soka barani Ulaya wameunga mkono mpango wa kuhamisha michuano ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar kuchezwa katika majira ya baridi baada ya kukubaliana kwamba haitawezekana michuano hiyo kuchezwa katika majira ya kiangazi kama ilivyo kawaida. Makamu wa rais wa Shirikisho la Soka Duiani-FIFA Jim Boyce alithibitisha kuwa jambo walilokubaliana katika mkutano huo ni kwamba Kombe la Dunia nchini Qatar haliwezi kuchezwa katika majira ya kiangazi. Hata hivyo Boyce aliongeza kuwa kila mtu amekubaliana na hilo lakini ni tarehe halisi ya kuhamisha michuano hiyo ndio hawajafikia maamuzi yake. Suala la michuano hiyo kuandaliwa majira ya kiangazi nchini Qatar limekuwa likizua mjadala mkubwa kutokana na joto kali katika kipindi hicho linaloweza kufikia nyuzi joto 50. Kamati ya Utendaji ya FIFA inatarajiwa kukutana Octoba 3 mwaka huu huko jijini Zurich, Switzerland ili kujadili mapendekezo ya kuhamisha michuano hiyo katika majira ya baridi.
No comments:
Post a Comment