Wednesday, October 23, 2013

NILIMUUZA BECKHAM KWASABABU ALITAKA "KUNIPANDA KICHWANI" - FERGUSON.

MENEJA wa zamani wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson amesema David Beckham alitakiwa kuondoka katika klabu hiyo kwasababu nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza alidhani yeye ni mkubwa kuliko meneja. Katika kitabu chake kipya kinachoelezea maisha yake ya ukocha, Ferguson amesema aligombana na Beckham baada ya kumkosoa kwa kiwango chake alichokionyesha katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Arsenal ambao walipoteza. Katika kitabu hicho Ferguson ameandika kuwa dakika ambayo mchezaji wa United atakapodhani yeye ni mkubwa kuliko meneja ni lazima aondoke na Beckham alidhani yeye ni mkubwa kuliko Ferguson ndio maana akamuuza. Ferguson pia alionyesha wasiwasi wake kuhusu mtindo wa maisha ya watu mashuhuri kufuatia nyota huyo kumuoa Victoria Adams aliyekuwa nyota wa kundi la muziki la Spice Girls nchini humo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa Beckham ndiye mchezaji pekee kati ya aliyowafundisha kuchagua maisha ya umaarufu na kitendo hicho hakikumfurahisha ndio maana akamuacha aondoke. Lakini Ferguson alimpongeza nyota huyo kwa mchango wake uliochangia mafanikio mengi ya United na kumtaja kama kioo cha watoto wote duniani. Katika kipindi chote cha miaka 26 aliyofundisha United, Ferguson alishinda mataji 38 na kufanikiwa kuwafundisha nyota kadhaa wakiwemo Beckham, Eric Cantona, Cristiano Ronaldo, Peter Schmeichel, Bryan Robson, Roy Kean, Jaap Stam na Ruud Van Nistelrooy.

No comments:

Post a Comment