Monday, October 28, 2013

PLATINI ATAKA NCHI 40 KOMBE LA DUNIA.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA, Michel Platini anataka michuano ya Kombe ya Dunia kuongeza timu kufikia 40 kuanzia mwaka 2018 ili kuruhusu nchi zaidi kwa upande wa bara la Afrika na Asia kushiriki michuano hiyo bila kupunguza timu kutoka bara la Ulaya. Kwasasa Ulaya inaingiza timu 13 kati ya 32 kwenye mashindano hayo ukilinganisha na tano za Afrika na nne au tano zingine kutoka Asia bara ambalo lina watu wengi zaidi ulimwenguni. Wiki iliyopita rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter aliandika kuwa Afrika na Asia wanastahili kuwa na wawakilishi zaidi katika michuano hiyo kwasababu wana vyama vingi zaidi vya uwakilishi ukilinganisha na Ulaya na Amerika Kusini. Platini ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuikwaa nafasi ya Blatter amesema kwa mahesabu aliyopiga zikiongezeka timu nane itabidi michuano hiyo iongezwe siku tatu zaidi kitu ambacho sio kibaya. Platini aliendelea kudai kuwa anakubaliana kwa asilimia mia moja na hoja ya Blatter lakini badala ya kupunguza timu kutoka bara la Ulaya ni kuongeza timu kufikia 40.

No comments:

Post a Comment