ZAMBIA imetoa vibali vya kukamatwa kwa wachezaji wake watatu waliokosa mechi ya kirafiki dhidi ya Brazil mjini Beijing China mchezo ambao nchi hiyo ilifungwa kwa mabao 2-0. Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC ilisisitiza kuwa wachezaji hao Rainford Kalaba, Stoppila Sunzu na Nathan Sinkala walijeruhiwa na kusababisha mgogoro kati ya Shirikisho la Soka la Zambia-ZFF na serikali yake. Baada ya wachezaji hao kufanyiwa uchunguzi jijini Lusaka, ZFF ikasisitiza kuwa bado wanaweza kusafiri kwenda China kwa mechi hiyo, lakini klabu ya Mazembe ambako wachezaji hao hucheza soka ya kulipwa ikawataka kurejea. Hatua hiyo ilisababisha serikali ya Zambia kuingilia kati kwa kuwapokonya wachezaji hao pasi zao za usafiri ili kuwazuia kwenda kuchezea klabu yao mjini Lubumbashi. Hata hivyo, wachezaji walifanikiwa kuvuka mpaka na wanaaminika kuwa nchini DRC. ZFF limeandikia barua Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, na kulalamika kuwa klabu ya Mazembe haikuwaruhusu wachezaji hao kushiriki majukumu yao ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment