Thursday, October 31, 2013

UEFA YAMSAFISHA MWAMUZI HATEGAN.

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limejiridhisha kuwa mwamuzi Ovidiu Hategan aliyechezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Manchester City na CSKA Moscow alifuata taratibu. Hatua hiyo imekuja kufuatia kiungo wa City Yaya Toure kulalamika kuwa alifanyiwa vitendo vya kibaguzi katika mchezo huo uliochezwa Octoba 23. Pamoja na UEFA kumsafisha mwamuzi lakini pia walitoa adhabu kwa CSKA kuchezwa bila ya mashabiki katika uwanja wao wa Khimki kwenye mchezo unaofuata wa michuano hiyo dhidi ya Bayern Munich Novemba 27 mwaka huu. Katika taarifa ya UEFA iliyotolewa katika mtandao wake imedai kuwa mwamuzi huyo alipopokea malalamiko alimfuata kamisaa wa mchezo kumuambia atoe tangazo uwanjani la kukanya tabia hiyo kama utaratibu unavyoelekeza. Kwa maana hiyo UEFA iliridhishwa na hatua alizofuata mwamuzi ingawa tatizo limeonekana kwa aliyekuwa msimamizi wa uwanja kwani hakutoa tangazo hilo baada ya kuona kelele hizo zimetulia.

No comments:

Post a Comment