Sunday, October 13, 2013

WAKALA WA BALE ACHUKIZWA NA UDAKU WA MAGAZETI.

WAKALA wa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale aitwae Jonathan Barnett amelishambulia gazeti la Marca la Hispania ambao lilitoa taarifa kuwa mteja wake anasumbuliwa na matatizo ya uti wa mkongo. Nyota huyo anayekipiga katika klabu ya Real Madrid bado hajacheza dakika zote 90 toka awe mchezaji soka ghali zaidi katika historia ambapo amecheza mechi tatu pekee katika kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na Carlo Ancelotti. Barnett alikuja juu na kutetea tuhuma hizo kuwa Bale ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili kutokana na majeraha ya misuli alishindwa vipimo vya afya kabla ya uhamisho wake ambao uligharimu kitita cha euro milioni 100. Barnett amesema alizungumza na mwandishi wa gazeti hilo na kumhakikishia kwamba tuhuma hizo hazina ukweli wowote lakini bado mwandishi huyo alitoa habari hiyo ya uongo. Wakala huyo amedai kuwa Bale alifaulu vipimo vya afya alivyofanyiwa Madrid kwa asilimia 100 na kama angekuwa na tatizo lolote klabu hiyo isingempa mkataba huo mnono.

No comments:

Post a Comment