MCHEZAJI nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani LeBron James amethibitisha kuwa yuko katika mazungumzo na David Beckham kwa ajili ya mipango ya baadae ya kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Marekani-MLS kutoka Miami. Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, ambaye aliweka kipengele cha kuwa na uwezo wa kununua timu katika mkkataba wake wakati aliposaini klabu ya Los Angeles Galaxy mwaka 2007, tayari ameshakutana na viongozi wa MLS Octoba kuangalia uwezekano wa kuanzisha timu huko Florida.
James, ambaye anamiliki hisa katika klabu ya Liverpool amethibitisha kuzungumza na Beckham kuhusu uwezekano wa kuirejesha MLS katika mji wa Miami na ana uhakika mpango wao huo utakuwa na mafanikio. James amesema Beckham amekuwa rafiki yake kwa miaka kadhaa iliyopita na pia anadhani itakuwa ni jambo zuri jiji hilo kuwa na timu yake ya soka. Mara ya mwisho jiji la Miami kuwa na timu MLS ilikuwa mwaka 2002 wakati timu Miami Fusion iliposhushwa daraja baada ya misimu minne pekee.
No comments:
Post a Comment