MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Croatia, Mario Mandzukic yuko katika hatari ya kukosa mechi tatu za hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani wakati Shirikisho la Soka Duniani-FIFA litakapotoa uamuzi kuhusiana na kesi ya kinidhamu kesho. Mbali na kesi ya nyota huyo, FIFA imedai pia kamati yake ya nidhamu itashughulikia kesi ya beki wa nchini hiyo Joe Simunic ambaye aliwaongoza mashabiki jijini Zagreb kuimba nyimbo zenye kauli mbiu za kimabavu baada ya Croatia kufuzu kwa kuifunga Iceland mwezi uliopita. Mandzukic anatarajia kukosa mechi moja ya ufunguzi ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Brazil baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Johann Gudmundsson wa Iceland katika mchezo baina ya timu hizo. Lakini kamati ya nidhamu ya FIFA inaweza kuongeza adhabu zaidi kama wakijiridhisha kuwa faulo iliyochezwa na nyota huyo ilikuwa ya kudhamiria. Mbali na kucheza na Brazil, Croatia pia itacheza na Cameroon na Mexico katika kundi A kwenye michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 12 mwakani.
No comments:
Post a Comment