Tuesday, December 10, 2013

MESSI, RONALDO, RIBERY KUCHUANA TUZO ZA BALLON D'OR.

SHIRIKISHO la soka Duniani-FIFA limetoa orodha ya wachezaji watatu watakaochuana katika kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa mwaka 2013 maarufu kama Ballon d'Or ambao ni Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Franck Ribery. Messi ameshinda mfululizo mara nne tuzo zilizopita, lakini safari hii ni Ronaldo anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa mpira wa dhahabu. Mshambuliaji huyo wa Real Madrid, amefunga mabao 32 tayari msimu huu kwa klabu na timu yake ya taifa, huku Messi kwa sasa yupo nje ya kikosi cha Barcelona kutokana na maumivu ya nyama. Mabao yake matatu aliyofunga peke yake, hat-trick wakati Ureno inaifunga 3-2 Sweden katika mechi maalum ya kufuzu Kombe la Dunia, yameongeza hamasa za watu kumpendekeza kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili katika historia yake. Ribery, aliyeiwezesha Bayern Munich kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kuishinda kabla ya Ronaldo kufanya mambo makubwa dhidi ya Sweden na FIFA ikaongeza muda wa kupigia kura washindani. Mshindi atatangazwa katika usiku wa hafla maalum ya Ballon d'Or mjini Zurich, Usiwis Januari 13, mwakani.

No comments:

Post a Comment