KOCHA wa timu ya taifa ya Urusi, Fabio Capello amefikia makubaliano ya kuongeza mkataba na nchi hiyo mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2018. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 alichukua nafasi ya Dick Advocaat Julai mwaka 2012 na kuisaidia nchi hiyo kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil akiwa amepoteza mechi mbili pekee katika kundi F la timu za Ulaya walilokuwepo. Mkataba wa sasa Capello ulikuwa umalizike baada ya michuano hiyo ya mwaka huu lakini ameongezewa mkataba mwingine mpya ambao utafikia tamati baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2018 ambayo Urusi itakuwa mwenyeji. Akihojiwa Capello amesema anamshukuru rais wa Umoja wa Soka wan chi hiyo, RFU pamoja na waziri husika wa michezo, Vitaly Mutko kwa kumuamini na kudai kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha anawapa furaha mashabiki wa Urusi. Urusi imepangwa katika kundi H sambamba na timu za Ubelgiji, Algeria na Korea Kusini.
No comments:
Post a Comment