KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania Vicente del Bosque amekiri kuwa ana wasiwasi kuhusu fikra za wachezaji wake wakati wakielekea katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika baadae mwaka huu nchini Brazil. Hispania ambao ni mabingwa wa Dunia na Ulaya walitandikwa mabao 3-0 katika mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka jana na Del Bosque amewaonya nyota wake kutobweteka na mafanikio waliyopata huko nyuma. Del Bosque amesema kuna wachezaji katika kikosi chake ambao wameshinda karibu kila kitu na wanaona vitu kwa jicho tofauti ukilinganisha na miaka mitano au sita iliyopita. Kocha huyo amesema jambo la msingi analowasisitizia ni kusahau mafaniko yaliyopita ili kuhakikisha wanarejesha makali yao. Del Aliendelea kudai kuwa wanakwenda katika Kombe la Dunia ambalo ni tofauti, nchi tofauti na bara tofauti hivyo wanatakiwa kwenda kule kwa nguvu ile ile kama ilivyokuwa Afrika Kusini mwaka 2010. Hispania inatarajiwa kukwaana na Uholanzi, Chile na Australia katika kundi B huku mchezo dhidi ya Uholanzi ukikumbushia fainali ya mwaka 2010 ambapo timu hizo zilikutana.
No comments:
Post a Comment