MSHAMBULIAJI nyota wa Colombia, Radamel Falcao hivi sasa anakimbizana na muda kwa kuwa fiti kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Juni mwaka huu nchini Brazil baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti jana. Madaktari waliomfanyia upasuaji mchezaji huyo wamempa zaidi ya asilimia 50 kwa 50 kwamba anaweza kupona kwa wakati na kushiriki michuano hiyo. Rais wa Colombia Juan Manuel Santos alimtembelea nyota huyo katika hospitali ya Trindade iliyopo jijini Porto Ureno wakati akitoka katika mkutano wa masuala ya kiuchumi uliokuwa ukifanyika huko Davos, Switzerland. Mara baada ya kumuona Santos amesema amemkuta nyota huyo katika hali nzuri na kuna mategemeo mazuri ya kupona kwa wakati kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia. Rais huyo aliongeza kuwa Colombia ina wachezaji wengi wazuri na kikosi imara lakini Falcao amekuwa alama ya timu ya taifa ya nchi hiyo. Nyota huyo anatarajiwa kuruhusiwa kutoka hospitalini Jumatatu na kuendelea na matibabu yake jijini Monaco, Ufaransa.
No comments:
Post a Comment