WANASOKA maarufu na wadau mbalimbali wa mchezo huo wameendelea kutuma salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha nguli wa zamani wa soka wa Ureno Eusebio aliyefariki kwa mshtuko wa moyo jana. Nyota huyo wa zamani wa klabu ya Benfica ambaye jina lake kamili ni Eusebio da Silva Ferreira alifunga mabao 733 katika mechi 745 alizocheza kama mchezaji wa kulipwa na kuwa mfungaji bora katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1966. Mojawapo ya wanamichezo maarufu waliotuma salamu zao za rambirambi ni kocha wa Chelsea raia wa Ureno Jose Mourinho ambaye alimuelezea Eusebio kama mchezaji wa kipekee ambaye hawezi kutokea wa aina yake. Mbali na Mourinho pia mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo naye alituma salamu zake akimuelezea nguli huyo kama baba wa soka ambaye uwezo wake uwanjani uliwavutia wengi katika kipindi hicho na mpaka sasa. Enzi zake Eusebio ambaye ni mzaliwa wa Msumbiji alifanikiwa kutwaa taji la michuano ya Ulaya akiwa na Benfica mwaka 1962 kabla ya kwenda na Ureno katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1966 iliyofanyika Uingereza na kufunga mabao tisa.
No comments:
Post a Comment