RAIS wa klabu ya Barcelona, Sandro Rosell ametangaza kujiuzulu rasmi wadhifa wake akidai kutishiwa maisha yeye pamoja na familia yake. Hatua hiyo ya Rosell imekuja wakati yeye na Barcelona wakiwa katika uchunguzi wa Mahakama Kuu ya Hispania kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za uhamisho wa Neymar kutoka Santos katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi mwaka jana. Rosell amesema kwa kipindi kirefu sasa familia yake pamoja naye wamekuwa wakiandamwa na vitisho vya kushambuliwa hatua ambayo ilimfanya kufikiria kama anaiweka familia yake katika hatari kwa kuendelea kuwa rais wa Barcelona. Tajiri huyo aliendelea kudai kuwa anadhani familia yake itafurahia uamuzi wake huo kwani umekuwa mjadala wa kipindi kirefu na baada ya kufikiria kwa makini. Nafasi ya Rosell sasa itashikiliwa na makamu wake Josep Maria Bartomeu mpaka hapo utakapoitishwa uchaguzi mwingine.
No comments:
Post a Comment