MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Manchester United, Wayne Rooney amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwaunga mkono wakati watakapopambana na Swansea City ili washinde na kumaliza uteja wa kupigwa mechi tatu mfululizo. United walijikuta wakichapwa na Tottenham Hotspurs katika mchezo wa ligi waliocheza siku ya mwaka mpya na kufuatia kutolewa katika Kombe la FA na Swansea kabla ya kukubalia kipigo kingine kutoka kwa Sunderland katika mchezo wa Kombe la Ligi mkondo wa kwanza. Timu hiyo kwa sasa iko nyuma ya vinara Arsenal kwa alama 11 ambapo wanaelekea katika mechi ya leo huku wakiwa na matumaini ya kushinda ili kuweza kumaliza katika nafasi nne za juu ili waweze kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao. Hatua ya Rooney kuwaangukia mashabiki wa United inakuja kufuatia timu hiyo kupoteza michezo yake minne waliyocheza katika uwanja wao wa nyumbani Old Traford msimu huu. Rooney amesema katika kipindi hiki kigumu wanahitaji zaidi kuungwa mkono na mashabiki ili waweze kurejesha makali yao na kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao zijazo.

No comments:
Post a Comment