Sunday, January 26, 2014

WAWRINKA BINGWA MPYA WA MICHUANO YA WAZI YA AUSTRALIA.

MCHEZAJI nyota wa tenisi Stanislas Wawrinka wa Switzerland amefanikiwa kumsimamisha kinara wa mchezo huo kutoka Hispania Rafael Nadal na kunyakuwa taji lake la kwanza la michuano ya wazi ya Australia katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Rod Laver Arena jijini Melbourne. Katika mchezo huo Wawrinka alitumia vyema udhaifu wa mpinzani Nadal ambaye alionekana kupata maumivu ya mgongo mapema katika mchezo huo na kumfunga kwa seti 3-1 zenye alama za 6-3 6-2 3-6 6-3. Wawrinka mwenye umri wa miaka 28 anakuwa mchezaji wa pili kutoka Switzerland kushinda taji la Grand Slam baada ya Roger Federer kufanya hivyo kwa kushinda mataji 17. Ushindi huo pia utampaisha Wawrinka ambaye kwasasa anashika nafasi ya nane katika orodha za ubora duniani, mpaka nafasi ya tatu katika orodha mpya zitakazotoka kesho akimshusha Andy Murray wa Uingereza aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment