MENEJA wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola amesisitiza kuwa Javi Martinez atapuuza taarifa kuwa anatakiwa na Real Madrid kwa ajili ya kuendelea kuichezea timu hiyo. Kiungo huyo mahiri alijiunga na Bayern akitokea Athletic Bilbao kwa ada ya paundi milioni 40 mwaka 2012 na ameendelea kubakia kuwa mchezaji aliyenunuliwa ghali zaidi katika Ligi Kuu nchini Ujerumani inayojulikana kama Bundesliga. Hata hivyo kumekua na tetesi kuwa nyota huyo atarejea nchini Hispania lakini Guardiola amesisitiza Martinez mwenye umri wa miaka 25 ataendelea kubakia Bayern katika kipindi chote atakachokuwa akiifundisha. Guardiola amesema hadhani kama uhamisho wa mchezaji huyo utawezekana kwasababu bado wanamhitaji kwa asilimia 100 katika kikosi chake. Kwa kipindi kirefu Martinez amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya kifundo cha mguu lakini hivi sasa anaonekana kupona na kuna uwezekano akarejeshwa katika kikosi cha kwanza.
No comments:
Post a Comment