MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amekiponda Chama cha Soka cha Uingereza, FA kwa kushindwa kumpa adhabu kiungo wa Manchester City Yaya Toure. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alionekana akimpiga teke Ricky van Wolfswinkel wa Norwich City katika mchezo baina ya timu hizo uliochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Carrow Road lakini hakupewa adhabu yoyote na mwamuzi Jonathan Moss. Jopo la maofisa wa FA walikubaliana kuwa Toure hakufanya kosa lolote lakini Mourinho anaamini kuwa jopo hilo linatoa ujumbe mbaya na unaweza kuwaongoza wachezaji kuendelea kufanya vitendo hivyo uwanjani. Mourinho amesema kama FA wameweka sheria kuwa hatua zinaweza kuchukuliwa kwa mchezaji hata kama mwamuzi hakuliona wanapaswa kuitumia sheria hiyo. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kama Toure hajafungiwa basi ujumbe uko wazi kuwa wachezaji wanaweza kufanya chochote uwanjani mradi wasionwe na mwamuzi.
No comments:
Post a Comment