MABINGWA wa soka wa Ubelgiji, Anderlecht wamemtimua kocha wao John va den Brom baada ya kupata kipigo cha tisa katika Ligi Kuu nchini humo msimu huu. Anderlecht walipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa OH Leuven inayoshika mkia katika msimamo wa ligi hiyo na kupelekea kuporomoka mpaka nafasi ya tatu huku wakiwa nyuma ya vinara Standard Liege kwa alama 12. Klabu hiyo kongwe iliyowahi kutamba barani ulaya miaka ya 70 na 80 pia walitolewa katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu kwa kuambulia alama moja. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo, imedai kuwa wameamua kusitisha mkataba na kocha huyo baada ya kuifundisha kwa karibu miaka miwili kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo. Taarifa iliendelea kudai kuwa imeamua kumpandisha kocha msaidizi Bisnik Hasi ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Albania ambaye aliwahi kuitumikia Anderlecht kati ya mwaka 2000 na 2006.

No comments:
Post a Comment