MFANYAKAZI wa ujenzi ameumizwa vibaya nchini Brazil baada ya kuanguka katika Uwanja wa Corinthians ambao utatumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia baadae mwaka huu. Jina la mfanyakazi huyo halikubainishwa wazi lakini kitengo cha zima moto cha jiji la Sao Paulo wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumkimbiza majeruhi hospitali. Imeripotiwa kuwa mfanyakazi huyo alianguka umbali wa mita nane na sasa yuko katika hali mbaya hospitali. Uwanja wa Corinthians umepangwa kutumika kwa ajili ya mechi sita za Kombe la Dunia ukiwemo mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Brazil na Croatia sambamba na ule wa Uingereza na Uruguay. Uwanja huo tayari umeshazua majanga kipindi cha karibuni kufuatia wafanyakazi Fabio Luis Pereira mwenye miaka 42 na Ronaldo Oliviera dos Santos mwenye miaka 44 wote kupoteza maisha katika tukio lilitokea Novemba mwaka jana. Pia kumekuwa ni vifo vingine vilivyotokea wakati wa ujenzi katika viwanja vya Amazonia uliopo Manaus na Mane Garrincha uliopo jijini Brasilia.
No comments:
Post a Comment