Monday, March 10, 2014

MAKUNDI YAIVA LIGI YA MABINGWA, NIGERIA NA GHANA VILABU VYAO VYASHINDWA KUFUZU.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika jana ilimaliza mechi zake za mzunguko wa pili kufuzu hatua ya makundi kwa viwanja mbali mbali barani Afrika kuwaka moto kwa mechi za mkondo wa pili. Macho na masikio jana yalikuwa huko jijini Alexandria, Misri ambako kulikuwa na mchezo uliowakutanisha wenyeji ambao pia ni mabingwa watetezi Al Ahly na Yanga ulioamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3 wenyeji wakiibuka kidedea. Katika mechi ya mkondo wa kwanza Al Ahly walijikuta wakiangukia pua kwa kulambwa bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam lakini walifanikiwa kusawazisha bao hilo katika mchezo wa pili na kufanya uweze kuamuliwa kwa mikwaju ya penati. Katika mechi hizo vigogo wa soka barani humu Nigeria na Ghana zilijikuta zikishindwa vibaya katika mechi za mkondo wa pili kwa vilabu vyao kushindwa kutinga mzunguko wa mwisho wa kufuzu katika hatua ya makundi. Klabu nyingine yenye jina kubwa barani Afrika Raja Casablanca ya Morocco nayo ilishindwa kutamba kutinga katika hatua ya timu 16 zitakazopita katika mchujo mwingine kabla ya kuingia rasmi hatua ya makundi ambapo mshindi wake ataliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia mwishoni mwa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment