HATIMAYE Chama cha Soka cha Misri kimethibitisha kuwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika kati ya Al Ahly na Yanga utachezwa Jumapili katika Uwanja wa Harras El-Hedoud uliopo jijini Alexandria. Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imekataa mechi kuchezwa jijini Cairo baada ya mashabiki wa Al Ahly wanaojulikana na kama Ultra Ahlwy kutangaza kuhudhuria mchezo huo ambao ulitakiwa kuchezwa bila ya mashabiki. Baada ya kugomewa kucheza jijini Cairo, maofisa wa timu hiyo waliangalia uwezekano wa kutumia uwanja uliopo katika mji wa El Gouna lakini kocha na wachezaji walipinga hivyo maofisa hao kuugeukia uwanja wa huo. Mkurugenzi wa EFA Tharwat Suweilem alithibitisha kuwa tayari wamepokea barua rasmi kutoka wizara ya mambo ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha usalama katika mchezo huo na wao kuipeleka kwa Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF pamoja na maofisa wa Yanga.

No comments:
Post a Comment