BAADA ya kumshinda katika tuzo za Ballon d’Or , sasa Cristiano Ronaldo amemshinda tena hasimu wake Lionel Messi kwa kuwa na mkwanja mrefu zaidi. Nyota huyo anayecheza klabu Real Madrid anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia paundi milioni 122 kwa mujibu ya orodha ya wachezaji matajiri iliyotolewa na mtandao wa Goal.com. Mkataba mpya wa miaka mitano wenye thamani ya paundi milioni 86.5 aliosaini na Madrid Septemba mwaka huu ndio uliompandisha Mreno huyo juu ya Messi ambaye anakadiriwa kuwa na utajiri wa paundi 120. Ukiacha Ronaldo na Messi katika nafasi ya kwanza na pili katika orodha hiyo, mshambuliaji wa Chelsea Samuel Eto’o yuko katika nafasi ya tatu akiwa na utajiri wenye thamani ya paundi milioni 70 na kufuatiwa na Wayne Rooney mwenye utajiri wa paundi milioni 69. Wengine wanaofuatia na thamani ya utajiri wao ni Kaka paundi milioni 67.5, Familia ya Neymar paundi milioni 66, Ronaldinho paundi milioni 64, Zlatan Ibrahimovic paundi milioni 57, Gianluigi Buffon paundi milioni 52 na Thierry Henry paundi milioni 47.

No comments:
Post a Comment