Friday, April 4, 2014

ANELKA AFUNGUKA KUHUSU ISHARA ALIYOTOA.

MSHAMBULIAJI mkongwe wa kimataifa wa Ufaransa, Nicolas Anelka amevunja ukimya juu ya ishara ya saluti ya kinazi aliyotoa na kudai kuwa amekuwa mhanga kwa jamii inayoamini inaonewa kila wakati. Anelka alifungiwa mechi tano na kutozwa faini ya paundi 80,000 na Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa ishara hiyo aliyoionyesha wakati akishangilia bao katika mchezo dhidi ya West Ham United uliochezwa Desemba mwaka jana. Mshambuliaji huyo aliandika katika mitandao ya kijamii mwezi uliopita kutangaza kuondoka kutoka klabu ya West Bromwich Albion ambao nao baadae walidai kumtimua. Anelka amesema ishara yake ilieleweka vibaya kwasababu hana rekodi yoyote na masuala ya kibaguzi wala hana tatizo na jamii ya kiyahudi hivyo hajui kwanini amekuwa mhanga kwa jambo ambalo hausiki nalo. Toka mwanzo Anelka amekuwa akijitetea kuwa alitoa ishara mahsusi kwa ajili ya rafiki yake mchekeshaji Dieudonne M’Bala M’Bala ambaye hutumia ishara hiyo katika kazi zake nyingi za uchekeshaji. Mchekeshaji huyo naye amezuiwa kuingia nchini UIngereza baada ya vipindi vyake kadhaa kufungiwa nchini Ufaransa kufuatia kusimamishwa kwa Anelka.

No comments:

Post a Comment