MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa kiungo wake Mesut Ozil atakuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Hull City Jumapili, wakati Abou Diaby naye akitegemewa kurejea mazoezini wiki hii. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani hakuwemo katika kikosi cha Arsenal toka walipofungwa bao 1-0 na Stoke City mapema mwezi Machi baada ya kuumia msuli wa paja, wakati Diaby yeye hajacheza mechi hata moja msimu huu kutokana na majeraha ya kuchanika msuli wa ndani ya goti la kushoto mwaka jana. Habari za Ozil kurejea zitakuwa njema kwa Wenger ambaye kwasasa anapambana kuhakikisha anamaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi huku pia akikabiliwa na fainali ya Kombe la FA dhidi ya hao hao Hull City. Akihojiwa mara baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham United jana usiku, Wenger amesema ni ahueni kubwa kwa Ozil kurejea uwanjani hususani katika kipindi ambacho wanakabiliwa na mechi muhimu.
No comments:
Post a Comment